Romans 4

Ibrahimu Alihesabiwa Haki Kwa Imani

1 aTuseme nini basi, kuhusu Ibrahimu baba yetu kwa jinsi ya mwili: yeye alipataje kujua jambo hili? 2 bKwa maana ikiwa Ibrahimu alihesabiwa haki kwa matendo, basi, anacho kitu cha kujivunia, lakini si mbele za Mungu. 3 cKwa maana Maandiko yasemaje? “Ibrahimu alimwamini Mungu na ikahesabiwa kwake kuwa haki.”

4 dBasi mtu afanyapo kazi, mshahara wake hauhesabiwi kwake kuwa ni zawadi, bali ni haki yake anayostahili. 5 eLakini kwa mtu ambaye hafanyi kazi na anamtumaini Mungu, yeye ambaye huwahesabia waovu haki, imani yake inahesabiwa kuwa haki. 6 fDaudi pia alisema vivyo hivyo aliponena juu ya baraka za mtu ambaye Mungu humhesabia haki pasipo matendo:
7 g“Wamebarikiwa wale
ambao wamesamehewa makosa yao,
ambao dhambi zao zimefunikwa.

8 hHeri mtu yule
Bwana hamhesabii dhambi zake.”

Haki Kabla Ya Tohara

9 iJe, huku kubarikiwa ni kwa wale waliotahiriwa peke yao, au pia na kwa wale wasiotahiriwa? Tunasema, “Imani ya Ibrahimu ilihesabiwa kwake kuwa haki.” 10 jJe, ni lini basi ilipohesabiwa kwake kuwa haki? Je, ilikuwa kabla au baada ya kutahiriwa kwake? Haikuwa baada, ila kabla hajatahiriwa. 11 kAlipewa ishara ya tohara kuwa muhuri wa haki aliyokuwa nayo kwa imani hata alipokuwa bado hajatahiriwa. Kusudi lilikuwa kumfanya baba wa wote wale waaminio pasipo kutahiriwa na ambao wamehesabiwa haki. 12 lVivyo hivyo awe baba wa wale waliotahiriwa ambao si kwamba wametahiriwa tu, bali pia wanafuata mfano wa imani ambayo Baba yetu Ibrahimu alikuwa nayo kabla ya kutahiriwa.

Ahadi Ya Mungu Hufahamika Kwa Imani

13 mKwa maana ile ahadi kwamba angeurithi ulimwengu haikuja kwa Ibrahimu au kwa wazao wake kwa njia ya sheria bali kwa njia ya haki ipatikanayo kwa imani. 14 nKwa maana ikiwa wale waishio kwa sheria ndio warithi, imani haina thamani na ahadi haifai kitu, 15 okwa sababu sheria huleta ghadhabu. Mahali ambapo hakuna sheria hakuna makosa.

16 pKwa hiyo, ahadi huja kwa njia ya imani, ili iwe ni kwa neema, na itolewe kwa wazao wa Ibrahimu, si kwa wale walio wa sheria peke yao, bali pia kwa wale walio wa imani ya Ibrahimu. Yeye ndiye baba yetu sisi sote. 17 qKama ilivyoandikwa: “Nimekufanya wewe kuwa baba wa mataifa mengi.” Yeye ni baba yetu mbele za Mungu, ambaye yeye alimwamini, yule Mungu anaye fufua waliokufa, na kuvitaja vile vitu ambavyo haviko kana kwamba vimekwisha kuwako.

Mfano Wa Imani Ya Ibrahimu

18 rAkitarajia yasiyoweza kutarajiwa, Ibrahimu akaamini, akawa baba wa mataifa mengi, kama alivyoahidiwa kwamba, “Uzao wako utakuwa mwingi mno.” 19 sIbrahimu hakuwa dhaifu katika imani hata alipofikiri juu ya mwili wake, ambao ulikuwa kama uliokufa, kwani umri wake ulikuwa unakaribia miaka mia moja, au alipofikiri juu ya ufu wa tumbo la Sara. 20 tLakini Ibrahimu hakusitasita kwa kutokuamini ahadi ya Mungu, bali alitiwa nguvu katika imani yake na kumpa Mungu utukufu, 21 uakiwa na hakika kabisa kwamba Mungu alikuwa na uwezo wa kutimiza lile aliloahidi. 22 vHii ndio sababu, “ilihesabiwa kwake kuwa haki.” 23 wManeno haya “ilihesabiwa kwake kuwa haki,” hayakuandikwa kwa ajili yake peke yake, 24 xbali kwa ajili yetu sisi pia ambao Mungu atatupa haki, sisi tunaomwamini yeye aliyemfufua Isa Bwana wetu kutoka kwa wafu. 25 yAlitolewa afe kwa ajili ya dhambi zetu, naye alifufuliwa kutoka mauti ili tuhesabiwe haki.
Copyright information for SwhKC